Mahakama Kuu Yamuamuru Harmonize Kulipa Sh113 Milioni kwa Benki ya CRDB

Dar es Salaam: Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imetoa amri kwa msanii maarufu wa Bongofleva, Rajab Abdul Kahali Ibrahim, maarufu kama Harmonize, kuilipa Benki ya CRDB Sh113 milioni kama sehemu ya deni la mkopo aliodaiwa pamoja na fidia.

Uamuzi huo umetolewa na Mahakama hiyo Agosti 2, 2024, kufuatia kesi ya madai iliyofunguliwa na Benki ya CRDB dhidi ya Harmonize kwa kushindwa kurejesha mkopo wa Sh300 milioni aliouchukua mwaka 2019. Jaji Cleophas Morris, ambaye alisikiliza kesi hiyo, aliamuru msanii huyo kulipa kiasi cha Sh103.18 milioni kama sehemu ya deni lililosalia na Sh10 milioni kama fidia ya hasara kwa benki hiyo.

Mahakama pia ilimuamuru Harmonize kulipa riba ya asilimia 18 kwa mwaka kwa deni hilo kuanzia tarehe aliyoshindwa kulipa hadi tarehe ya hukumu. Vilevile, Harmonize anatakiwa kulipa riba ya asilimia saba kwa mwaka kwa jumla ya kiasi anachotakiwa kulipa, kuanzia tarehe ya hukumu hadi atakapokamilisha malipo yote, pamoja na gharama za kesi.

Kesi hiyo ya biashara namba 151 ya mwaka 2023 ilisikilizwa upande mmoja baada ya Harmonize kupuuza wito wa mahakama kuwasilisha utetezi wake wa maandishi na kutofika mahakamani kujitetea licha ya kupewa wito mara nne kwa nyakati tofauti.

CRDB ilimpatia Harmonize mkopo wa Sh300 milioni mnamo Oktoba 10, 2019, kwa ajili ya kununua vifaa vya muziki, kuanzisha studio, na kufadhili uzalishaji wa muziki wake. Mkopo huo ulitakiwa kurejeshwa ndani ya miezi 36, lakini msanii huyo alishindwa kutimiza masharti hayo na hakumaliza kulipa mkopo huo.

Harmonize alijaribu kuomba benki hiyo kupunguza kiwango cha marejesho ya mkopo hicho kutoka Sh10.8 milioni hadi Sh3.3 milioni kwa mwezi, ombi ambalo lilikubaliwa lakini hakuweza kutimiza malipo hayo kwa wakati.

Baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa na benki hiyo, Mahakama iliridhika kuwa CRDB imethibitisha madai yake kwa kiwango kinachohitajika kisheria na hivyo kutoa amri hiyo dhidi ya Harmonize.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here