Yanga Bingwa ya Harmonize Yaondolewa YouTube kwa Kuiga Wimbo wa Innoss’b

Wiki iliyopita, Harmonize aliachia wimbo wake mpya uitwao “Yanga Bingwa,” ambao ulikuwa maalum kwa kusherehekea mafanikio ya klabu ya Yanga. Mashabiki wa klabu hiyo na wapenzi wa muziki wa Tanzania waliupokea wimbo huo kwa shangwe kubwa.

Mara ya kwanza, Harmonize alitumbuiza wimbo huo Jumapili, Agosti 4, 2024, katika siku ya Mwananchi ‘Yanga Day’. Mashabiki walikusanyika kwa wingi kusherehekea mafanikio ya msimu uliopita wa klabu hiyo. Wimbo huo uliachiwa rasmi kwenye majukwaa yote ya kidigitali, ukiwemo YouTube, na kwa muda mfupi ukapata umaarufu mkubwa.

RELATED: Harmonize – Yanga Bingwa

Hata hivyo, siku chache baada ya kuachiwa, wimbo huo ulikutana na changamoto kubwa. Video ya “Yanga Bingwa” iliondolewa kwenye YouTube channel ya Harmonize kutokana na ripoti kutoka kwa msanii wa Kongo, Innoss’b. Kwa mujibu wa taarifa kwenye link ya video hiyo, Innoss’b alidai kuwa Harmonize aliiga wimbo wake.

Sababu halisi ya ripoti hiyo bado haijafahamika wazi, na kuacha maswali mengi kwa mashabiki. Innoss’b ni msanii maarufu barani Afrika na amepata mafanikio makubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Harmonize, ambaye jina lake halisi ni Rajab Abdul Kahali, ni msanii maarufu wa Bongo Fleva, akijulikana kwa nyimbo zake nyingi zilizopendwa. Amejipatia umaarufu kutokana na sauti yake ya kipekee na uwezo wa kuandika nyimbo zinazovutia na kuhamasisha.

Hii ni mara ya pili kwa Harmonize kukumbwa na kisa cha kuondolewa kwa wimbo wake YouTube. Mwanamuziki wa Kenya aliripotiwa kuuondoa wimbo mpya wa Harmonize, ‘Sherehe’. Hapo awali, mtayarishaji wa muziki wa Kenya, MagixEnga, aliwahi kuondoa wimbo wa Harmonize, ‘Uno’, kutoka YouTube.

Mashabiki wa Harmonize na Yanga wanasubiri kwa hamu kuona hatua atakazochukua msanii huyo katika kurejesha wimbo huo kwenye YouTube. Kwa sasa, mashabiki wanaendelea kusikiliza wimbo huo kupitia majukwaa mengine ya kidigitali kama Boomplay, ambapo bado unaendelea kufanya vizuri na kushika nafasi ya kwanza kwa nyimbo zinazotafutwa zaidi Boomplay Tanzania kwa siku nne mfululizo.